ZAHERA AOMBA MSAMAHA YANGA, KULIKONI,,,

Pamoja na kuwepo kwa mbwembwe nyingi za maneno ya kuwafedhehesha baadhi ya viongozi wa Yanga zilizokuwa zikitolewa na Mwinyi Zahera, imebainika kuwa kocha huyo aliomba msamaha kiaina na mabosi wa timu hiyo.

‘Zahera alifutwa kazi na Yanga Jumanne iliyopita na uongozi huo kwa madai ya kutoridhishwa na mwendo wa ufundishaji wake ndani ya kikosi hicho hasa baada ya kupoteza kwenye michezo miwili ya Kombe la Shirikisho Afrika, dhidi ya Pyramids ya Misri.

Baada ya hapo Zahera alianza ratiba ya kuzunguka kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuzungumza mambo kibao kuhusiana na timu hiyo hata yale ya siri.

Kikizungumza na Championi Jumamosi chanzo cha habari kilieleza kuwa, kabla Zahera hajaondoka nchini kuelekea DR Congo kwenye majukumu ya timu ya taifa ambapo yeye ni kocha msaidizi, alilazimika kwenda kwenye ofisi za Yanga kuchukua barua yake ya kufutwa
kazi na baadhi ya stahiki zake.

Alipofika huko akakutana na mabosi wakubwa wa timu hiyo hapo ndipo akajikuta akiomba msamaha huku akiweka wazi kuwa alikuwa na mhemuko baada ya kusitishiwa kazi.

“Zahera amepatikana ile mbaya katumia mdomo wake kubwabwaja kwenye vipindi mbalimbali vya radio kabla hajaondoka lakini mwisho wa siku amejikuta akiwa mdogo baada ya kutakiwa kwenda kuchukua stahiki zake makao makuu ya klabu.

“Akiwa hapo alikutana na baadhi ya mashabiki na wanachama na kujikuta wakimchunia jambo lililosababisha aombe msamaha kwa kila mtu aliyemkuta klabuni hapo.

“Nakumbuka wakati anakuja alishushwa kwenye gari lake lakini cha ajabu hali aliyoikuta siyo kama zamani, ambapo alizoea kupokelewa kwa shangwe lakini siku hiyo hakushobokewa jambo lililomfanya ashituke na kuanza kuomba msamaha, maana wakati anafika ofisini alimkuta Kaimu Katibu Mkuu, Thabit Kandoro.

“Pia alikutana na viongozi wengine mbalimbali akiwemo Mkurugenzi wa Biashara na Masoko, Robert Kabeya, Simon Patrick ambaye ni Mkurugenzi wa Sheria na Wanachama wa klabu hiyo na mwenyekiti, Dk. Mshindo Msolla.

“Hao wote aliwaomba msamaha kwa maneno aliyoyatoa kisha wakaagana naye na kumpatia barua yake ya kumfuta kazi na mambo mengine yote,” kilisema chanzo hicho ambacho kilikuwa eneo la tukio

Post a Comment

0 Comments