WAKULIMA WA PAMBA SIMIHU KUPATA BIMA YA MAZAO


Shirika la Bima la Taifa (NIC)linatarajia kuanza kutoa huduma za bima ya mazao kwa wakulima wa pamba katika Wilaya ya Meatu na Maswa Mkoani Simiyu, ambapo wakulima watakuwa na uwezo wa kukata bima katika zao la pamba itakayomkinga dhidi ya majanga ukame,mvua zilizozidi kiasi , mafuriko, moto pori ,magonjwa na wadudu wasiothibitika.

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Bima ya mazao kutoka Shirika la Bima la Taifa (NIC),  Bw. Prosper Peter wakati akitoa mafunzo kwa  viongozi, wataalam wa Kilimo na ushirika mkoa wa Simiyu yaliyoandaliwa na NIC  yaliyofanyika Novemba 07, 2019 Mjini Bariadi kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja juu ya Bima ya Mazao inayotarajiwa kutolewa kwa  wakulima wa pamba mkoani Simiyu.

“Huduma ya bima ya mazao  itaanza kwanza na kumkinga mkulima dhidi ya majanga kama vile ukame , mvua zilizozidi kiasi , mafuriko, moto pori,magonjwa na wadudu wasiothibitika na itakatwa kwa pamoja kwa hiyo tutakuwa tunakinga mtaji wa mkulima aliouwekeza katika kilimo,” alisema Peter.

Aidha, Peter amesema pamoja na bima kukinga mtaji wa mkulima katika uzalishaji, NIC kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo itaendelea kuboresha na kuongeza wigo wa huduma za bima ya mazao kwa kuangalia mahitaji ya wakulima wa pamba kwa wakati husika  ikiwemo suala la bei.

Awali akifungua mafunzo Katibu Tawala mkoa wa Simiyu,Bw, Jumanne Sagini amesema wakulima wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa pembejeo, mvua iliyozidi hivyo Bima itawahakikishia kupata fidia pale wanapopata hasara inayosababishwa na changamoto hizo na kusisitiza viongozi na wataalam kutoa ushirikiano kwa NIC wanapotekeleza

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi amesema kuwa ujio wa bima ya mazao ni wa msingi hivyo ni vema NIC ikatoa bima kwa mahitaji/changamoto ambayo ni ya kipaumbele katika eneo fulani kwa kuwa changamoto za wakulima zinatofautiana, huku akitolea mfano kwa mkoa wa Simiyu kuwa ukame hauna athari sana kwenye zao la pamba.

Afisa kilimo wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Bibi. Suzana Sabuni amesema  kuwa ni vyema bima hiyo ijikite kwenye vipaumbele vya wakulima kutokana na mazao wanayolima ikiwa ni sambamba na kuwapata uhuru wakulima  kuchagua bima wanayoitaka

Naye afisa ushirika kutoka wilaya ya Itilima Heri Muhina ameshauri kuwa katika upande wa majanga ni vyema bima ilenge kuwasaidia katika majanga ya moto ambayo yamekuwa yakitokea kwenye baadhi ya maghala ya vyama vya ushirika (AMCOS) pindi wakulima wanapokuwa wamehifadhi pamba yao.

Akifunga kikao hicho mkuu wa wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amesema kuwa ni vyema utekelezaji huo uanze mapema kuelekea msimu mpya wa kilimo wa mwakani 2019/ 2020 na kusisitiza wakulima wapate taarifa sahihi kwa wakati ili waweze kuifahamu vizuri kabla ya utekelezaji.

Post a Comment

0 Comments