Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: “Mtu huwa katika dini ya rafiki yake, basi mmoja wenu achunguze ni yupi anayemfanya kuwa rafiki yake.”[1]
Imam Ali (a.s.) amesema: “Aliye madhubuti ni yule mwenye kupata kheri kwa urafiki wake, kwani hakika mtu hupimwa kupitia rafiki yake.”[2]
Imam Ali (a.s.) amesema: “Urafiki una majuto ila kwa walio wachamungu.”[3]
Imam Ali (a.s.) amesema: “Rafiki wa mtu ni dalili ya akili yake.”[4]
Imepokewa kuwa Sulayman (a.s.) alisema: “Msimhukumu mtu kwa chochote mpaka mchunguze husuhubiana na nani, kwani hakika mtu hujulikana kupitia wenzi wake na marafiki wake, na hunasibishwa kwa sahiba zake na wapambe wake.”[5]
Kumjaribu rafiki:
Imam Ali (a.s.) amesema: “Kumwamini kila mtu kabla ya kumjaribu ni dalili ya kushindwa.”[6]
Imam Ali (a.s.) amesema: “Tangulizeni majaribio na fanyeni juhudi katika uchunguzi wakati wa kuchagua ndugu, la sivyo utalazimika kufanya urafiki na waovu.”[7]
Imam Ali (a.s.) amesema: “Akili za watu hujaribiwa kwa mambo sita: Urafiki, muamala, utawala, kuvuliwa madaraka, utajiri na ufakiri.”[8]
Imam Ali (a.s.) amesema: “Watu hawajulikani ila kwa majaribio, basi mjaribu mkeo na wanao katika ghaibu yako, rafiki yako katika msiba wako, mwenye ukaribu na wewe katika ukata wako na mwenye mapenzi na wewe wakati wa kutengana naye, ili ujue ni ipi nafasi yako kwao.”[9]
Imam As-Sadiq (a.s.) amesema: “Msimuone mtu kuwa ni rafiki mpaka mumjaribu kwa mambo matatu: “Mghadhibishe uone ghadhabu zake je zitamtoa kwenye haki hadi kwenye batili, na wakati wa dinari na dirhamu (Dola na shilingi), na mpaka usafiri naye.”[10]
Aina za marafiki:
Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) amesema: “Zama za mwisho kutakuwa na watu, wao ni marafiki kwa nje na maadui kwa ndani.” Akaambiwa: ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hiyo inakuwaje?’ Akasema: ‘Hiyo ni kwa kupendana wao kwa wao na kuogopana wao kwa wao.”[11]
Imam Ali (a.s.) amesema: “Marafiki zako ni wa aina tatu na maadui zako ni wa aina tatu: Marafiki zako ni rafiki yako, rafiki wa rafiki yako na adui wa adui yako. Na maadui zako ni adui yako, adui wa rafiki yako na rafiki wa adui yako.”[12]
Imam Al-Baqir (a.s.) amesema: “Mtu mmoja huko Basra alisimama kwa kiongozi wa waumini na kumwambia: ‘Ewe kiongozi wa waumini tupe habari kuhusu ndugu.’ Akasema: ‘Ndugu wana namna mbili: Ndugu wa kweli na ndugu wa uongo. Ama ndugu wa kweli wao ndio uwezo, rafiki, ndugu na mali.
Ukiwa na imani na ndugu yako basi jitolee kwake mali yako na mwili wako, msafie nia aliyemsafia nia na mfanyie uadui aliyemfanyia uadui, mfichie siri yake na aibu yake na mdhihirishie wema. Na jua ewe muulizaji hakika wao ni wachache kuliko madini ya kibiriti chekundu. Ama ndugu wa uongo, hakika wewe utapata ladha yako (manufaa) kutoka kwao, hivyo usilikatishe hilo kutoka kwao, na wala usitafute yaliyo nyuma ya hayo kutoka katika dhamiri zo, na wape ucheshi wa uso na utamu wa ulimi kama walivyokupa.”[13]
Imam As-Sadiq (a.s.) amesema: “Ndugu wana namna tatu: Mmoja ni kama chakula ambaye anahitajika kila wakati, naye ni yule mwenye akili. Wa pili ni sawa na ugonjwa naye ni yule mpumbavu. Na wa tatu ni sawa na dawa naye ni yule mwerevu.”[14]
Marafiki bora:
Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.): “Ndugu bora ni yule mwenye kukusaidia katika amali za Akhera.”[15
Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.): “Aliye bora kati ya ndugu zako ni yule anayekusaidia katika kumtii Mwenyezi Mungu, anayekuzuia kumwasi Mwenyezi Mungu na anayekuamuru kumridhisha.”[16]
Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.): “Mbora kati ya ndugu zenu ni yule mwenye kuwazawadieni (kukujulisheni) aibu zenu.”[17]
Alipoulizwa: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ni yupi aliye mbora kukaa naye? Akasema: “Ni yule ambaye kumtazama kwake kunawakumbusha Mwenyezi Mungu, kuongea kwake kunawaongezea elimu na matendo yake yanawakumbusha Akhera.”[18]
Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.): “Wanafunzi wa Isa walimuuliza: ‘Ewe roho wa Mwenyezi Mungu, tukae na nani?’ Akasema: ‘Yule ambaye kumtazama kwake kunawakumbusha Mwenyezi Mungu, kuongea kwake kunawaongezea elimu, na matendo yake yanawaraghibisha Akhera.”[19]
Imam Ali (a.s.) amesema: “Ndugu bora ni yule aliye mchache wa hadaa katika nasaha.”[20]Imam Ali (a.s.) amesema: “Ndugu bora ni yule ambaye mapenzi yake ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.”[21]
Imam Ali (a.s.) amesema: “Ubora wa kila kitu ni upya wake, na ndugu bora ni wa zamani.”[22]
Imam Al-Baqir (a.s.) amesema: “Mfuate anaekuuliza ilihali akikunasihi, wala usimfuate anayekuchekesha ilihali akikuhadaa.”[23]
Imam As-Sadiq (a.s.) amesema: “Shikamana na rafiki wa zamani kwani kila mpya hana ahadi na uaminifu, wala dhima na mkataba. Na chukua tahadhari sana dhidi ya yule uliye na imani naye sana, kwani watu ni maadui wa neema.”[24]
Imam Al-Askar (a.s.) amesema: “Ndugu aliye bora kwako ni yule aliyesa- hau makosa yako na akakumbuka ihsani yako kwake.”[25]
Imam Hasan (a.s.) amesema: “Mtume (s.a.w.w.) aliulizwa: ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ni yupi rafiki bora?’ Akajibu: ‘Rafiki ambaye unapomkumbuka Mwenyezi Mungu anakusaidia na unapomsahau anakukumbusha.’ Wakamwambia: ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, tuonyeshe aliye mbora kwetu ili tumfanye rafiki na mtu wa kukaa naye.’ Akasema: ‘Ndio, yule ambaye akitazamwa Mwenyezi Mungu hukumbukwa.”[26]
Haki ya mwenzi wako:
Imam Zaynul-Abidina (a.s.) amesema: “Ama haki ya mwenzi wako uliyekaa naye ni uwe mpole kwake na kumfanyia insafu katika utamshi wa lafudhi. Usisimame toka ulipokaa ila kwa idhini yake, na aliyekaa kwako anaruhusiwa kusimama toka kwako bila idhini yako. Sahau makosa yake na hifadhi kheri zake na wala usimsikilizishe ila kheri.”[27]
0 Comments