Tanzania na Burundi wamesaini makubaliano ya kuwarejesha Wakimbizi 2000 kwa kila wiki nchini mwao kuanzia Oktoba Mosi, 2019.

Wakimbizi hao waliopo katika Kambi ya Nduta na Mtendeli wanatarajiwa kusafirishwa kuelekea katika nchi yao ya asili kutokana na amani iliyopo katika nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, na Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Burundi, Pascal Barandagiye tayari wamesaini makubaliano hayo ambayo watahakikisha wakimbizi wote waliopo katika kambi hizo wanarejeshwa nchini mwao bila kukwamishwa na mtu au shirika lolote.

Akizungumza na waandishi wa habari, mjini Kigoma, Waziri Lugola amesema kuwa makubaliano hayo yataanza rasmi Oktoba mosi na wakimbizi hao watakuwa wanarejeshwa nchini mwao na kupata mapokezi makubwa na Serikali ya Burundi.

“Tunataarifa wapo baadhi ya watu, mashirika ya kimataifa wanawarubani wakimbizi wakiwatangazia kuwa Burundi haina amani, jambo ambalo si la kweli, nchi hiyo ina amani na wakimbizi wanapaswa kurejea nchini mwao,” amesema Lugola

Lugola ameongeza kuwa, atawachukulia hatua kwa watakaokwamisha zoezi hilo la kuwasafirisha wakimbizi hao, kwa kuwa Serikali ya Tanzania imeamua kuwapa watu wao ili waende wakaijenge nchi yao.

“Natoa kauli hii sio kuwatisha au kutishia Nyau, bali nasema, Serikali ya Magufuli haiwezi kuchezewa na mtu yeyote, hivyo tutawakamata wanaowarubuni, wanaowashawishi wakimbizi wasiende nchini mwao,”amesisitiza Lugola.

Wiki iliyopita, katika mkutano wa hadhara katika Kambi ya Nduta, baadhi ya Wakimbizi walisema wanawekewa vikwazo na kucheleweshwa na baadhi ya watendaji wa mashirika ya wakimbizi kambini humo wakati wanapoomba kujiandikisha kurejeshwa kwao