Muziki sio vita. Muziki ni burudani. kinachoendelea ndani ya lebo kubwa ya muziki nchini, WCB kinahuzunisha wala si burudani kama watu wanavyodhani. Habari kuwa, “Konde boy” kung’atuka kutoka WCB zilipaswa kuchukuliwa kwa mtazamo chanya si kama wengine wanavyofikiri.

Rajabu Abdul Kahali maarufu kama “Harmonize” ni msanii ambaye hivi sasa amekonga nyoyo za washabiki wengi wa muziki barani Afrika na si Tanzania kama wengi wanavyodhani. Si ajabu sana kwa level aliyofikia kuanzisha lebo yake ya muziki, ambayo ataweza kusimamia kazi zake pamoja na wasanii watakao ungana naye jinsi anavyotaka yeye bila ya kuwa na usimamizi wa mtu mwingine.


Pia, tukumbuke: ni asili ya mwanadamu kupenda uhuru zaidi ya kitu chochote kile. Mtoto akikua mzazi hana budi kumuacha mtoto akatengeneze maisha yake jinsi anavyotaka yeye. Kipindi kama hiki kikifika, hakuna mzazi anayechukia kumuona mwanaye anakwenda kujitegemea bali humtakia kheri na kumpatia baraka.

Soko la muziki hivi sasa Tanzania limekuwa kwa kasi. Hivi sasa wasanii wa bongo flava nchini wanasikika mbali zaidi ya mipaka ya Afrika. Ukuaji wake unadhihirisha lakini haujafika kwenye zile levo za nchi kama Nigeria na Afrika Kusini kwa barani Afrika.

Ukienda Nigeria, utakutana na lebo za muziki kubwa sana ukilinganisha na hizi za kwetu nchini. Bila ya kupepesa macho ni wazi WCB ndio lebo ambayo angalau ukisema kuna lebo za muziki hapa nchini utaitaja. Hizi nyingine, ni lebo pia lakini hazijafika kwenye hadhi ya kulinganisha na lebo kama: Marvin Dynast, X3M Music, DMW (Davido music worldwide), Chocolate City na nyingine nyingi.


Hapa Tanzania, wasanii wameamka kutoka usingizini, usingizi ambao uligubikwa na ujinga pamoja na ukosefu wa maarifa. Ni jambo la kupongezwa sana pale unapoona wasanii wanatengeza lebo zao, nakuanza kusimamia kazi pamoja na biashara zao za muziki. Mfano, wasanii kama Fid Q, Diamond, Ally Kiba, Vanessa Mdee, Madee na wengine wengi hivi sasa wanamiliki lebo za muziki zinazosimamia kazi zao pamoja na zile za wasanii wao waliowasaini.

Konde boy kufungua lebo yake ya muziki na kaachana na bosi wake Diamond pamoja na lebo ya WCB, Kwani kuna ubaya gani pale mtoto uliyemlea na akawa mtu mzima akiomba kwenda kujitegemea? Ni bongo tu ambapo utasikia mtu akiondoka chini ya mtu flani utasikia wana ugomvi. Wasanii kama Rosa Ree, Chin Beez, Wildad walipo achana na “Industry” ya Nahreel unasikia eti, demu wa Nahreel anazingua. Maprodyuza wakiondoka “Switch” ya Q Rocka, utasikia “Switcher Baba” anazingua kinouma!

Bwana mdogo S2Kizzy alipoondoka “Switch records” ya Q Rocka, wadau wengi wamechukulia kuondoka kwake kama vita; sasa ni lini tungetarajia kuona “Pluto Republic” rekodi lebo, ambayo mwaka huu imetengeneza historia ya muziki nchini? Hivi sasa ‘Switcher Baba’ anajivunia kuwa baba kwa watayarishaji mbalimbali ambao walipita katika mikono yake na baadae wakaenda kutengeneza lebo zao.


WCB ni moja, lini tutapata nyingine kama Konde akiendelea kuwepo pale? natarajia kuwaona wakina RayVany, Lava Lava, Queen Darlin na wakina Romy Jones wakitengeneza lebo zao miaka ya hivi karibuni alafu washirikiane na WCB kutengeneza pesa kwenye game hii.


Walikuwepo wakina 50 Cent, Buster Rhymes, Eve, Missy Elliot, The Game ndani ya lebo ya ‘Aftermath’ inayomilikiwa na nguli wa muziki nchini Marekani, Dr. Dre na baadae wote wakaondoka, hakuna msanii nchini Marekani ambaye hana ndoto kuwepo ndani ya ‘Aftermath’ lakini leo hii tunazungumzia lebo kama G Unit, Flipmode, Goldmind kama matunda ya wasanii hawa kuachana na Aftermath na baadae kuanzisha za kwao.


Wapo wengine wanaenda mbali kutengeneza uhasama baina ya watu kitu ambacho katika kiwanda cha muziki ni makosa. Muziki ni sehemu ya burudani, huko mbele tunaona kwenye masumbwi wakina Pacquiao na Mayweather wanapigana alafu baadae unawaona viti virefu wakipongezana baada ya kutengeneza pesa zao lakini, hapa Bongo kuna wajinga eti wanasambaza chuki zisizo na maana kitu ambacho kwenye muziki akikubaliki.