Upande wa mashtaka katika kesi ya kutekwa kwa mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘Mo’ umedai kuendelea na taratibu za kuwatafuta watuhumiwa watano ili kuwaunganishwa katika kesi hiyo.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Agosti 20, 2019 na wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.



Amesema upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na wanaendelea kuwatafuta watuhumiwa hao watano raia wa Msumbiji na Afrika Kusini.



Watuhumiwa hao ni Henrique Simbue, Daniel Berdardo Manchice,Issac Tomu na Zacarious Junior wote raia wa Msumbiji na Phila Tshabalala raia wa Afrika Kusini.



Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 3, 2019.

Mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ni Dereva taksi, Mousa Twaleb (46).

Katika kesi ya msingi, Twaleb anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Mei Mosi, 2018 na Oktoba 10, 2018 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na Johannesburg, nchini Afrika Kusini.



Anadaiwa kwa makusudi alitoa msaada wa kutendeka vitendo vya jinai, uhalifu wa kupangwa kwa lengo la kujipatia faida.



Katika shitaka la pili, Twaleb anadaiwa Oktoba 11, 2018 katika maeneo ya Hoteli ya Colloseum iliyopo wilayani Kinondoni, pamoja na watu wengine ambao hawajafikishwa mahakamani, walimteka nyara Mo kwa nia ya kumhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.



Katika shitaka la tatu, Simon amedai Julai 10, 2018 katika maeneo ya Mbezi Beach Wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa alitakatisha fedha kiasi cha Sh8 milioni wakati akijua fedha hizo ni zao la kosa la kushiriki genge la uhalifu.