MWANDISHI wa habari, Joseph Gandye, ambaye ni Mhariri wa Uzalishaji Maudhui, Msimamizi Msaidizi wa Watetezi TV amekamatwa na polisi akituhumiwa kutoa taarifa za uongo kupitia mitandao ya kijamii.
Gandye alikamatwa jana, Agosti 22, 2019, baada ya kupigiwa simu na askari aliyejitambulisha kwa jina la Godfrey Mkude ambaye alimtaka mwandishi huyo kwenda kituo cha polisi Urafiki kwa ajili ya mahojiano.
Baada ya kuchukuliwa maelezo chini ya wakili Jones Sendodo, dhamana yake ilikataliwa kwa maelezo kwamba amri ya kumkamata imetoka Iringa, hivyo kituo cha polisi Urafiki wao wanamhifadhi na baadaye atapelekwa Iringa kwa ajili ya taratibu zingine.
Kwa mujibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) mnamo Juni 17, 2019, waandishi wa habari wa kituo cha runinga cha mtandaoni (Online TV) cha Watetezi TV walipokea taarifa ya kuwepo kwa vitendo vya udhalilishwaji wa watuhumiwa katika Kituo cha Polisi Mafinga mkoani Iringa.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Gandye alifunga safari hadi mkoani Iringa kwa ajili ya kufuatilia habari hiyo kwa kufanya uchunguzi wa kutosha na mnamo Agosti 09, 2019 waliripoti tukio la ukatili wa askari wa jeshi la polisi katika Kituo cha Polisi Mafinga mkoani Iringa katika mitandao yake (Facebook, Twitter na Youtube Channel).
Katika tukio hilo inadaiwa kuwa vijana sita (majina yao yanahifadhiwa) wakazi wa Mafinga walikamatwa na kuteswa na maofisa kwa jeshi la polisi na inadaiwa kuwa walipigwa na kulazimishwa kulawitiana wao kwao wakiwa kituoni.
Watuhumiwa hao sita walikamatwa na jeshi la polisi mnamo mwezi Mei 19, 2019 na kushikiliwa kwa takribani siku 10 katika kituo hicho cha Mafinga, ambapo inadaiwa kuwa walipigwa na kulazimishwa kulawitiana wao kwa wao mbele ya maofisa wa jeshi la polisi kituo cha Mafinga wakati wakifanyiwa mahojiano.
Baada ya sehemu ya kwanza ya tukio hilo kuripotiwa Agosti 09, 2019 kuhusu ukatili huo, jeshi la polisi mkoani Iringa kupitia kwa Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC), ACP Juma Bwire, lilikanusha taarifa hiyo na kudai kuwa ni uongo unaosambazwa mitandaoni kwa lengo la kulidhalilisha jeshi la polisi na kuichafua serikali kwa jumla.
Agosti 22, 2019 Gandye aliyechapisha habari hiyo ametakiwa kuripoti Kituo cha Polisi Urafiki, Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano.
Gandye ambaye alipigiwa simu majira ya saa 05.20 alifika kituoni hapo na kusubiri kwa zaidi ya saa mbili.
Mwandishi huyo alihojiwa mbele ya Wakili Jones Sendodo kwa tuhuma za kuchapisha habari za uongo mtandaoni kinyume na Sheria ya Makosa ya Mtandao.
Wakati Gandye yuko Urafiki, polisi kutoka Iringa wanafanya mipango ya kumsafirisha kwenda mkoani huko.
0 Comments