Mfanyabiashara mmoja kutoka eneo la Juja Farm, Kaunti ya Kiamba nchini Kenya anasononeka baada ya mkewe wa miaka 26 waliyejaliwa watoto watano kunyakuliwa na mchungaji aliyesimamia harusi yao.

John Kanyua ameshindwa kuelewa ni vipi mchungaji aliyewasaidia wakati wa ndoa yao, hata akatia saini cheti chao cha harusi, alitembea na mkewe wa zaidi ya miongo miwili.

Mwanamume huyo hakutambua kuwa mchungaji huyo alikuwa akimezea mate mkewe, Leah Wambui, kwa miaka hiyo yote licha ya baadhi ya waliohudhuria harusi yao kubaini ukweli huo.

Hayo yote yalianza wanandoa hao walipoanza kuhudhuria kanisa la pasta huyo eneo la Juja Farm.

Na baada ya kupendezwa na mchango wao kanisani, mchungaji huyo alimteua Leah kuwa naibu wake katika Kanisa hilo, jambo lililofanya mke wa mchungaji kuingiwa na wasiwasi.

“Nilipinga uteuzi, lakini alinipuuzilia mbali. Nilimkabili Leah na kumwonya dhidi ya kucheza na mume wangu. Alionekana asiye na hatia, na nikakubali,” alisema Agnes Wangivi, mke wa mchungaji.

Wazazi wa Leah sasa wamewasiliana na Kanyua wakimtaka akubali warejeshe mahari aliyotoa kwao ili kutoa nafasi kwa harusi mpya ya binti yao, lakini mwamume huyo amekataa. Mchungaji huyo pia amewaambia watoto wake kwamba, anapanga kuoa mke mwingine na kwamba ametengana na mama yao.